Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama
cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amenusurika kifo na
mtu mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Mikidadi, ambaye yupo
mahututi katika Hospitali ya Temeke, baada ya kushambuliwa na watu
wanaodaiwa kuwa na mzozo wa ardhi eneo la Kurasini, jijini Dar es
Salaam.
Mchungaji Mtikila alikumbwa na mkasa
huo Ijumaa wiki iliyopita baada ya kufika katika eneo hilo kwa nia ya
kutaka kuwaondoa watu hao wa familia tatu tofauti ambao wanaishi katika
eneo hilo.
Kipigo hicho ambacho kimemsababishia
majeraha ya kisogoni na hata kushonwa nyuzi tatu kichwani, kuvimba
usoni na maumivu makali mwilini yalitokana na kipigo kutoka kwa familia
mbili tofauti zinazoishi katika eneo hilo ambao wanapinga kuhama.
Pia katika sakata hilo, Mtikila anadai
kupoteza simu mbili, pesa taslimu Sh400,000 na Dola za Marekani 2,000
na siku ya tukio na alifika hapo akiwa ameongozana na watendaji wa
Dawati la Msaada wa Kisheria katika taasisi yake ya Liberty Fund
International.
Kamanda wa Polisi Temeke, Engbert
Kiondo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa wanalifanyia
uchunguzi na taarifa kamili itatolewa kesho Jumanne.
“Ni kweli suala hilo limeripotiwa hapa
na tunalifanyia uchunguzi na kesho Jumanne nitatoa taarifa rasmi kwa
waandishi wa habari,” alisema Kiondo.
Mtikila alisema, mara baada ya kufika
eneo hilo, alikwenda katika nyumba ya kwanza na kuwakuta walinzi ambao
walikubali na kuondoka katika eneo hilo kwani tayari notisi walikuwa
nayo na walikuwa wanatambua kuwa wanatakiwa kuondoka.Alisema baadaye
walikwenda katika nyumba ya pili ambayo anaishi mtu mmoja aliyemtaja
kwa jina la Rubein Sanga ambaye hata hivyo vitu vyake vingi akuwa
amekwisha vihamisha.
Alisema wakiwa mbele ya nyumba hiyo
gari la polisi lilifika na wakiwa hawana hili wala lile vijana ambao
anawataja kuwa ni wa Sanga walianza kuwashambulia kwa kutumia nondo na
kila aina ya silaha za jadi.
“Walinipiga sana hadi nikapoteza fahamu
na wakawa wanasema huyo Mtikila bebeni na mumchome moto, walitaka
kuniua kwani walinikwida tai hadi ikakatika,” alisema.
Na kuitaja pia familia ya Evelyne Mboya
kuwa ilishiriki kuwashambulia. Alisema wakati vurugu zinaendelea,
ndipo akatokea mmoja wa jirani wanaoishi katika eneo hilo aliyemtaja
kwa jina la Mikidaki: “Yule bwana alipojaribu kunitetea kuwa
nisiendelee kupigwa alipigwa nondo kichwani na akaanguka na
alishambuliwa hadi kuzirai na hajapata fahamu hadi leo,” alisema.
Mchungaji Mtikila alisema alikuwa
ameambatana pia na walinzi wawili (mabaunsa), wafanyakazi wa dawati
lake la msaada wa kisheria lililopo chini ya taasisi yake ya Liberty
Fund International na mmiliki halali wa eneo hilo, Omar Salum Muhsin
ambaye pia alijeruhiwa mkononi kwa nondo.
Mtikila aliwataja wafanyakazi wake
waliojeruhiwa kuwa ni Hemed Wendo na Gray Mhando na akiwa amezirai
alibebwa na kupandishwa katika gari hadi Kituo cha Polisi Chang’ombe
ambako yeye na wenzake walifunguliwa jalada kwa shtaka la kuingia
isivyo halali katika eneo la watu wengine.
No comments:
Post a Comment