DVD YA MUNGU HABADILIKI YA MESS JACOB CHENGULA

Tuesday, January 28, 2014

HIVI NDIVYO MWINJILISTI ALIVYOMUUA MKEWE KWA KUMCHINJA KAMA KUKU

YULE Mwinjilisti wa Kanisa la Angilikana lililopo Kijiji cha Gama Makaani wilayani Bagamoyo, Pwani, Elikia Daniel (35) aliyemuua mkewe Mboni Patrick (28) kwa kumchinja kikatili naye kujinyonga, simulizi yake inashangaza.

Baada ya mauaji hayo, waandishi wa Uwazi walikwenda kwenye kijiji hicho kilichopo kilomita 100 kutoka jijini Dar es Salaam na kukutana na ndugu, jamaa, marafiki wa marehemu wote sanjari na uongozi wa kijiji.

MWANZO WA MKASA
Wakisimulia kwa masikitiko, wakazi wa kijiji hicho walisema siku ya tukio, Mwinjilisti Elikia na mkewe, Mboni walikwenda msituni kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa wa biashara. Walikuwa wameongozana na mtoto wao wa miaka (12) ambaye jina halikupatikana mara moja.

Baada ya kufika msituni, simulizi inasema, majira ya saa tatu asubuhi, mwinjilisti huyo alimtaka mwanaye huyo kurudi nyumbani kupika.
“Yule mtoto alipika chakula na kukiweka kwenye ‘hotipoti’ kwa ajili ya kuwapelekea wazazi. Alikwenda msituni akiwa ameambatana na mtoto wa jirani ambaye ni rafiki yake.

Waombolezaji wakiwa msibani.

WAZAZI HAWAPO
“Alipofika msituni, mahali alipowaacha wazazi wake hakuwakuta, akawaita kwa muda mrefu, baba, mama lakini ukimya ulitawala eneo lile.

“Katika juhudi za kuwasaka huku na kule, mtoto alishangaa kuona damu nyingi imetapakaa eneo lile na aliposogea akashangaa kuuona mkono wa mama yake ukiwa umetokeza nje huku mwili wake umefunikwa na magogo kwenye tanuri walilokuwa wakitumia kuchomea mkaa,” alisema ndugu mmoja wa marehemu Mboni aliyeomba hifadhi ya jina lake.

WATOTO WAKIMBIA KIJIJINI KUSEMA
Simulizi inazidi kuweka wazi kwamba, baada ya kuona hali hiyo, watoto hao huku wakilia walikimbilia kijijini ambapo waliwaambia watu walichokutana nacho msituni.
Wanakijiji walikukusanyika na kwenda eneo la tukio kushuhudia mwili wa mwanamke huyo.

MSAKO WAANZA
Kwa vile wawili hao waliachwa msituni na mtoto wao, wanakijiji waliamini kwamba, Elikia ndiye aliyefanya mauaji hayo, wakaanza kumsaka.
Walitembea umbali mrefu, wakafika mahali na kukuta nguo za mwinjilisti barabarani, waliposogea sehemu yenye miti iliyoshonana ndipo walipouona mwili wa Elikia ukining’inia mtini. Hakuacha ujumbe wowote.

NINI CHANZO?
Akizungumza kuhusu mauaji hayo, mwenyekiti wa eneo hilo, Ali Thabiti alisema kwa jinsi alivyopata taarifa kutoka kwa majirani, chanzo cha mauaji hayo ni fedha za mkaa. Mwinjilisti alikuwa akidaiwa fedha na mkewe lakini alikuwa akimzungusha kumlipa.

Alisema mgogoro wa marehemu hao ulikuwa wa muda mrefu, walishapelekwa mpaka kanisani kusuluhishwa, mwinjilisti alikubali ana makosa na kuahidi kwamba atangemlipa mkewe fedha za mkaa wake wa magunia mia moja alizokuwa akimdai.

“Usiku wa kuamkia siku ya tukio, mtoto alisema alimsikia baba yake akimwambia mama yake kuwa atamuua na kweli akamuua asubuhi iliyofuata,” alisema jirani mmoja.

UNAWEZA KUAMINI HII?
Vyanzo mbalimbali kijijini hapo vilieleza kuwa, mwinjilisti huyo aliwahi kudaiwa kumuua mtu (jina halikupatikana) huko Kigoma kwa kutumia nondo ambayo alimpiga nayo kichwani.

KUMBE MKE ALIKUWA MJAMZITO?
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwa eneo la tukio wakati daktari alipofika kuupima mwili wa marehemu Mboni, taarifa ilitoka kwamba mwanamke huyo alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu wakati anauawa.

NI MAUAJI YA KUTISHA
Mwili wa marehemu Mboni ulikutwa ukiwa na majeraha mengi, kubwa zaidi ni la shingoni kwani mumewe alimchinja kama kuku.

MWINJILISTI AZIKWA NA SANDA YA KIROBA
Baada ya polisi kufika eneo la tukio na daktari kufanya uchunguzi, wanakijiji walifikia uamuzi kwamba mwanamke azikwe eneo hilohilo ulipokutwa mwili wake, mwinjilisti alizikwa chini ya mti aliojinyongea, tena mwili wake ukiviringishwa kwenye kiroba. Wote walizikwa bila majeneza na miili yao iliharibika.

ASKOFU MOKIWA AMKANA MWINJILISTI
Uwazi lilizungumza na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentine Mokiwa (zamani alikuwa askofu mkuu Tanzania) ambaye alikana marehemu Elikia kuwa mwinjilisti wa kanisa hilo.

“Si kweli. Anglikana hatuna mwinjilisti huyo. Nimesoma kwenye vyombo vya habari kuhusu madai hayo, waandishi hawakuchunguza vizuri,” alisema Askofu Mokiwa.

No comments:

Post a Comment