DVD YA MUNGU HABADILIKI YA MESS JACOB CHENGULA

Saturday, July 12, 2014

MATUKIO KATIKA PICHA:WINGU JEUSI LATANDA MSIBA WA SISTA ANNA, DAYOSISI YA KUSINI

Msiba wa sista Anna Peterson umeibua simanzi si kwa familia yake tu bali kwa wananchi wa wilaya ya Makete mkoani Njombe alipokuwa akifanya kazi za kijamii tangu ujana wake.

Hayo yamebainika wakati wa ibaada maalum ya kumkumbuka iliyofanyika hii leo katika kanisa la KKKT usharika wa Amani Bulongwa, ibaada iliyoongozwa na baba askofu wa dayosisi ya kusini kati Levis Sanga, Askofu Mstaafu Dkt. Solomon Swallo na Askofu Mstaafu Shadrack Manyiewa pamoja na msaidizi wa askofu Philemon kahuka.


Sista Anna Enzi za uhai wake.

Akihubiri katika ibaada hiyo maalum Askofu Mstaafu Shadrack Manyiewa amesema marehemu alikuwa akifanya kazi zake kwa mkono wa dayosisi ya kusini kati tangu enzi za ujana wake bila ubaguzi ingawa yeye alikuwa mzaliwa wa nchi ya Sweeden.

Amesema amemfahamu toka 1969 na hadi anafikwa na umauti alikuwa akisaidia watoto yatima, wajane, wagane na walemavu wote na hata wasiojiweza na kusisitiza kuwa kanisa haliwezi kumsahau kamwe.

Akielezea historia ya marehemu Askofu mstaafu Dkt Solomon Swallo amesema Sista Anna alikuwa akifanya kazi zake kwa kujituma bila kujali ugumu wa kazi uliokuwepo kwa kipindi hicho hasa ubovu wa barabara na ugumu wa kuwafikia wananchi kutokana na tabu ya usafiri.

Askofu mstaafu Manyiewa akihubiri ibadani hapo.

Dkt Swallo amesema alikuwa akisisitiza kuwa Mungu ndiye aliyemtuma kufanya kazi Bulongwa Makete na si Binadamu hivyo haoni shida kutumikia jamii ya Makete toka ujana hadi uzee wake.

Askofu mstaafu Dkt Solomon Swallo.


Dkt Nicodemas Kikoti.

Kwa upande wake Kaimu Mganga mkuu hospitali ya Bulongwa Dkt Nicodemas Kikoti amesema marehemu pia alikuwa akifanya kazi na hospitali hiyo pamoja na jamii ikiwemo kusomesha watoto yatima kutoka shule ya awali mpaka vyuo, kuwajengea nyumba wasiojiweza, kuhudumia wajane, kusaidia vifaa vya umeme pamoja na kujenga makao ya kituo cha watoto yatima Bulongwa.


Mch. Dkt Phares Ilomo.

Naye Mch. Dkt Phares Ilomo kutoka chuo Kikuu cha Iringa amesema yupo tayari kuandika kitabu cha kuelezea historia ya marehemu Sista Anna kwa kushirikiana na viongozi wengine wa kanisa na washarika kuchangia gharama ili kitabu hicho kichapishwe na kuzalishwa kwa faida ya vizazi vijavyo ikiwemo kukiweka katika maktaba ya chuo chake.

Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais mazingira Dkt Binilith Mahenge ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Makete akitoa salamu za rambirambi amesema marehemu alikuwa akifanya shughuli ambazo kimsingi zilitakiwa kufanywa na serikali hivyo wema wake kwa jamii ya Makete hauna mfano.


Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais mazingira Dkt Binilith Mahenge ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Makete akitoa salamu za rambirambi.

Amesema njia pekee ya kumuenzi ni kufanya yale aliyoyapenda huku akisisitiza kuwa serikali itashirikiana na kanisa kuendeleza kazi zote alizoziacha Sista Anna.


Askofu wa dayosisi ya kusiki kati Levis Sanga.

Askofu wa dayosisi ya kusiki kati Levis Sanga ametangaza tarehe 26 Juni kila mwaka kuwa ni siku maalum kikanisa ya kumkumbuka marehemu sista Anna hivyo jamii inashauriwa kufika kwenye kituo cha watoto yatima Bulongwa kwa ajili ya kuwatembelea na siku hiyo itakuwa ikifanyika ibaada maalum kwa ajili ya marehemu.

Sista Anna Peterson amefariki Juni 26 mwaka huu nchini Sweeden alipokwenda kwa ajili ya matibabu na amezikwa leo hii nchini humo, na hapa Makete alikokuwa akiishi toka ujana wake imefanyika ibaada maalumu ya kumkumbuka.

Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Sista Anna Peterson, Amen.

Habari/Picha Na Edwin Moshi, Makete

No comments:

Post a Comment