WATU wanaodaiwa kuwa ni wa imani ya Freemason wametua ndani ya ibada
katika Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Mchungaji Kiongozi
Josephat Gwajima, Uwazi lina ‘ei tu zedi’ ya tukio hilo.
Baadhi ya vitu vilivyokutwa kanisani kwa Gwajima.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Freemason hao wawili waliingia kwenye ibada hiyo iliyofanyika Februari 23, mwaka huu ndani ya kanisa hilo lenye makao makuu yake katika Viwanja vya Tanganyika Peckers, Kawe jijini Dar wakiwa na mfuko wa rambo wenye vitu mbalimbali vikiwa na alama zao.
GWAJIMA MADHABAHUNI
Habari zilidai kwamba wakati neno likiendelea kunenwa na Mchungaji Gwajima, watu hao walifunua mfuko huo ambapo baadhi ya waumini waliokuwa karibu yao walihoji kulikoni kuwa kwenye ibada na vitu vyenye viashiria ya Freemason.
Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima.
“Wengine tulishangaa sana kwani baadhi ya vitu vilionekana kuwa na thamani kubwa, tukadhani labda wameleta zawadi kwa mtumishi wa Mungu (Gwajima),” kilisema chanzo hicho ambacho kinaabudu katika kanisa hilo.
MFUKO WANASWA NA WALINZI
Mtiririko wa tukio hilo unazidi kuwekwa wazi kwamba, haraka sana walinzi wa kanisa hilo walifika eneo lenye mfuko huo na kuunasa huku watu walioingia nao wakipotea au kujichanganya miongoni mwa waumini wengine.
WASIWASI WATANDA
Kufuatia tukio hilo, baadhi ya waumini wa kanisa hilo walipozungumza na Uwazi baada ya ibada kumalizika walisema wanaamini watu hao walifika kanisani hapo kwa nia mbili, kujisalimisha au kuzijaribu nguvu za Gwajima ambaye ni maarufu kwa kuibua misukule.
Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima akiongoza ibada.
MFUKO WENYE VITU
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa, ndani ya mfuko wa watu hao kulikutwa saa ya rangi ya fedha, pete ya dhahabu, cheni 2 za fedha, bangili, fulana nyeupe na shati jeusi, vyote vikiwa na picha zenye alama mbalimbali za Freemason kama mafuvu, nyoka na bikari.
“Lakini mimi naamini wale watu nia yao hasa ilikuwa kumjaribu mtumishi wa Mungu ambaye ni kinara wa kuwarudisha watu waliokufa katika mazingira ya mazingara (misukule),” kilisema chanzo kimoja na kujitambulisha kwa jina moja la Isaya.
IMANI KWA GWAJIMA YAKAZIWA
“Mimi ninavyomjua Gwajima sidhani kama wangefanikiwa, ni vigumu sana. Kuna majambazi waliwahi kujaribu kumuua lakini waliambulia patupu, wakapigwa na upepo wa kisurisuri, sembuse Freemason? Ninachokijua mimi watamjaribu lakini hawataweza,” kilisema chanzo kingine.
UWAZI MZIGONI, WALINZI WAWA MBOGO
Wakati sakata hilo likiendelea, mmoja wa waandishi wa Uwazi alipata taarifa ambapo aliwahi tukio hilo na kujaribu kupiga picha lakini mlinzi mmoja (jina tunalo) alimkataza licha ya kufanya jitihada kubwa.
Mlinzi huyo alimnyang’anya kamera mwandishi wetu na kuishikilia kwa muda huku akitishia kufuta picha zote hata kama hazikuwa za tukio hilo.
GWAJIMA KIMYA
Baada ya kuinyaka ishu hiyo nzima, Uwazi lilitumia siku tano kumsaka Mchungaji Gwajima ili kupata mtazamo wake juu ya tukio hilo ambalo huenda ni la kwanza kwenye kanisa hilo la kiroho jijini Dar es Salaam lakini bila mafanikio kutokana na kukwamishwa na wasaidizi wake.
Awali, ilikuwa Februari 25, mwaka huu ambapo hakupatikana kanisani kwake na hata kwa njia ya simu.
Baada ya kumkosa mtumishi huyo kwa kutopokea simu, Uwazi lilimtumia ujumbe wa simu (SMS) na kumuuliza kuhusu tukio hilo na ikiwezekana kukutana ambapo alijibu kwamba alikuwa kwenye kikao cha viongozi wa Kikristo, Kurasini jijini Dar, hivyo asingeweza kuonana na wanahabari.
Ijumaa ya Februari 28, mwaka huu, waandishi wa gazeti hili walitumia saa tano kumsubiri Gwajima kanisani kwake bila mafanikio.
MSIKILIZE MSEMAJI WAKE
Baadaye msemaji wa kanisa hilo, Mchungaji Yeconia Bihagaze alipoulizwa juu ya sakata hilo aliliambia gazeti hili kuwa, matukio kama hayo hutokea mara kwa mara licha ya kuchukua muda mrefu ikilinganishwa na hili la juzikati.
“Mambo ya Freemason kujisalimisha hapa mbona ni ya muda sana! Mimi naona kama yamepitwa na wakati, tukio hilo unalolisema mimi sijalisikia. Kanisa letu ni kubwa, mambo mengine ni madogomadogo hivyo siyo lazima yafike kwenye uongozi wa juu.
“Kwa nini msiandike misukule tunaowafufua hapa kila siku? Kwa nini msichukue matukio makubwa kwenye mtandao wa kanisa letu? Ninyi wanahabari wakati mwingine huwa mnatuvunjia heshima ndiyo maana huwa tunaamua kuwapotezea,” alisema Mchungaji Bihagaze.
Chanzo cha habari: Vituko vya Mtaa
No comments:
Post a Comment